Wednesday, October 12, 2016

VIONGOZI WA SERIKALI MWIKO KUHUDHURIA KILELE CHA MWENGE KWA KULIPANA POSHO.

BOFYA HAPA CHINI KUONA MAAJABU YA LEO

RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli ameagiza viongozi wote wa Serikali walioalikwa kuhudhuria sherehe za Kilele cha Mbio za Mwenge wa Uhuru,kutohudhuria bali waendelee kuwajibika katika maeneo yao.
 
Ametoa agizo hilo kwa viongozi hao wa serikali kutohudhuria sherehe za kilele hicho ambacho kitaifa zitakazofanyika tarehe 14 Oktoba, 2016 katika Wilaya ya Bariadi Mkoani Simiyu,na ambao walishalipwa fedha ya posho na safari kwa ajili hiyo, wazirejeshe.

Taarifa iliyotolewa leo tarehe 12 Oktoba, 2016 Ikulu Jijini Dar es Salaam na Katibu Mkuu Kiongozi Balozi John Kijazi imeeleza kuwa Rais Magufuli ametoa maagizo hayo ikiwa ni utekelezaji wa azma ya Serikali ya awamu ya tano ya kubana matumizi yasiyo ya lazima na kuelekeza rasilimali nyingi katika shughuli za maendeleo ya nchi.

Viongozi waliotajwa kutakiwa kufuta safari zao za kwenda Bariadi ni pamoja na Wakuu wote wa Mikoa, Wakuu wote wa Wilaya, Wakurugenzi wote wa Mamlaka za Serikali za Mitaa, Mameya na Wenyeviti wote wa Halmashauri za Majiji, Manispaa, Miji na Wilaya pamoja na watumishi ambao huambatana nao wakiwemo madereva na wasaidizi wao ambao kwa idadi hufikia takribani 1,500.

Kwa kuwa sherehe za Kilele cha Mbio za Mwenge wa Uhuru huambatana na Maadhimisho ya Siku ya Kumbukumbu ya Muasisi wa Taifa na Baba wa Taifa Hayati Mwalimu Julius Kambarage Nyerere aliyefariki dunia miaka 17 iliyopita, agizo hilo limewataka Viongozi wote wa Mikoa na Wilaya kubaki katika maeneo yao ya kazi na kujiwekea utaratibu wa jinsi ya kuienzi siku hiyo.

Aidha, Rais Magufuli ameagiza Wilaya zote ambazo zimefanya vizuri katika shughuli za maendeleo wakati Mwenge ulipokuwa katika maeneo yao, zitambuliwe kwa kutangazwa rasmi katika siku ya kilele cha Mbio za Mwenge na kwamba zawadi zilizoandaliwa zitapelekwa kwa wahusika kwa utaratibu utakaoelekezwa na Mamlaka inayohusika kutoa zawadi hizo.

Hata hivyo Dkt. Magufuli ameelekeza kuwa kutokana na umuhimu wa Mwenge wa Uhuru kwa Taifa, Viongozi wote wa Serikali ya Mkoa wa Simiyu na Wilaya zake pamoja na wananchi wote wa mkoa huo wajitokeze kwa wingi na kushiriki katika sherehe za kuzima Mwenge wa Uhuru siku hiyo ya tarehe 14 Oktoba, 2016.

Mgeni Rasmi katika sherehe za kuzima Mwenge wa Uhuru atakuwa Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe. Dkt. Ali Mohamed Shein.

KUONA VIDEO MPYA BOFYA HAPA CHINI