Wednesday, October 5, 2016

SHINYANGA YAKABILIWA NA UPUNGUFU WA DAMU KWA WATOTO.

BOFYA HAPA CHINI KUONA MAAJABU YA LEO



 IMEFAHAMIKA kwamba pamoja na mkoa wa Shinyanga kuwa ni miongoni mwa mikoa nchini inayopata mazao mengi ya chakula kila msimu wa kilimo,huku jamii yake ikionekana na maumbo makubwa,lakini inakabiliwa na tatizo la upungufu wa damu kwa watoto.

Tatizo hilo ambalo limekuwa sababu ya kuwepo kwa vijana wengi waliodumaa,limeelezwa kutokea kwa watoto wengi mkoani humo kutokana na jamii yake kutozingatia lishe bora kwa wakazi wake imesababisha tatizo la udumavu na upungufu wa damu kwa watoto,mkoani humo.  

Mganga mkuu wa Mkoa wa Shinyanga, Dr. Ntuli Kaporogwe,ameyabainisha hayo kwenye mdahalo uliohusu matumizi ya chakula na lishe, ambapo alisema licha ya wakazi mkoani humo kuonekana  na maumbo makubwa,lakini asilimia 71 ya watoto wanamatatizo ya upungufu wa damu.

Dr. Kaporogwe alisema tatizo hilo la damu linachangia  udumavu wa afya kutokana na wazazi wengi kutozingatia matumizi ya chakula chenye lishe pamoja na kuwa na chakula cha kutosha lakini hakitumiwi kwa kuzingatia matumizi halisi ya chakula kwa binadamu.

Alisema sababu nyingine inayochangia kuwepo kwa tatizo hilo ni kutokana na jamii hiyo kukabiliwa  na changamoto kubwa juu ya uelewa wa matumizi ya vyakula vyenye madhara mwilini,ambapo asilimia 70 ya chumvi inayouzwa Mkoani Shinyanga haina madini joto, hali ambayo inaleta madhara kwenye ubongo wa binadamu kuanzia akiwa mtoto mdogo.

Akizungumza katika mdahalo huo; Afisa lishe Mkoa wa Shinyanga, Mariam Mwita,alisema tatizo la udumavu kwa watoto chanzo chake kinaanzia kwa mama mjamzito,kutozingatia lishe wakati wa ujauzito hali ambayo inachangia kuzaliwa mtoto akiwa na hali hiyo.

Mwita alisema tatizo hilo limekuwa likichangiwa na mfumo dume uliojengeka kwenye jamii kwamba mwanaume ndio mwenye mamlaka ya kupanga lishe bila kumsikiliza mwanamke anapokuwa anaeleza hali ambayo inachangia tatizo kuwepo kubwa mkoani Shinyanga tofauti na mikoa mingine ya hapa nchini

Aidha Mwita alisema pamoja na kuwepo idadi kubwa ya watoto wenye upungufu wa damu pia kuna tatizo kubwa la utapiamlo na ugonjwa wa kuhara kwa watoto hali ambayo alipendekeza Halmashauri zote Mkoani Shinyanga kuwa na mikakati wa kushirikisha idara zote zinazohusika na chakula kukabiliana na tatizo la lishe

Nae Mratibu wa Mpango huo wa chakula na lishe, kutoka Shirika la HUHESO FOUNDATION, Juma Mwesigwa,alisema mpango mkakati wa kupambana na tatizo la lishe Tanzania unatekelezwa na zaidi ya mashirika mia tatu chini ya mwamvuli wa shirika mama la PANITA.

Mwesigwa ambaye pia ni Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la  HUHESO FOUNDATION alisema katika kanda ya Ziwa Magharibi,inayojumuisha mikoa mitatu ya Shinyanga,Kagera na Geita kuna jumla ya mashirika manane mwanachama wa shirika mama la PANITA,yanayojishughulisha na mapambano ya kuondoa tatizo hilo.


KUONA VIDEO MPYA BOFYA HAPA CHINI