HATIMAYE mjadala wa Bunge kutooneshwa matangazo yake moja kwa moja umefungwa jana baada ya Wabunge wa Chama Cha Mapinduzi(CCM),kuibuka kidedea kwa kuunga mkono maamuzi hayo ya serikali.
Wabunge hao wa CCM, waliwazidi wenzao wa upinzani
kwa kura za sauti “Siyooooo” kuikataa hoja ya kutaka matangazo ya Bunge
kurushwa moja kwa moja ‘live’ na televisheni,iliyowasilishwa na Mbunge wa Jimbo la Malindi(CUF);Ally Salehe.
Maamuzi hayo yalifikiwa baada ya Bunge kukaa kama kamati kupitisha bajeti ya Ofisi ya Rais (Tamisemi
na Utumishi na Utawala Bora) na kuzua mvutano mkali uliosababisha bajeti
hiyo ipitishwe kwa utaratibu wa wabunge kutohoji kitu chochote
(guillotine).
Wakati hoja yao hiyo ikipingwa kila kona, tangu
kuanza kwa Bunge la Bajeti, wabunge hao wa upinzani sasa wamebuni mbinu
mpya ya kujirekodi wenyewe wakati wakichangia mijadala mbalimbali
bungeni na kurusha sauti zao kwenye mitandao ya kijamii na kupeleka
sauti hizo kwenye redio zilizopo katika maeneo ya majimbo yao.
Mbunge
wa Malindi (CUF), Ally Salehe ndiye aliyeibua hoja hiyo akitaka kushika
mshahara wa waziri kwa maelezo kuwa kuzuia Bunge kurushwa ‘live’ ni
kinyume na utawala bora na haki ya kupata habari.
Hoja hiyo
iliungwa mkono na Mbunge wa Iringa Mjini (Chadema), Mchungaji Peter Msigwa,
Masoud Abdalla Salim (Mtambale-CUF), Rose Kamili (Viti Maalumu
-Chadema), Ester Matiko (Tarime Mjini – Chadema) na Mussa Mbarouk (Tanga
Mjini - CUF).
Wabunge wa CCM waliopewa nafasi na Mwenyekiti wa
Bunge, Andrew Chenge kuchangia hoja hiyo ni Peter Serukamba (Kigoma
Kaskazini), Kangi Lugola (Mwibara), Hawa Ghasia (Mtwara Vijijini) pamoja
na Waziri Ofisi ya Rais - Utumishi na Utawala Bora, Angela Kairuki.
Baada ya Salehe kutaka ufafanuzi wa kina huku akisisitiza kuwa uamuzi
huo unakiuka Katiba ya nchi na haki ya kupata habari, Kairuki alisema
kwa mujibu wa Ibara ya 18 na 100 ya Katiba zinazozungumzia uhuru wa
kupata habari, uamuzi huo ni sahihi na hakuna mwananchi aliyenyimwa
taarifa.
Maelezo hayo yalipingwa na Salehe, safari hii
akifafanua kuwa matangazo ya Bunge yanarekodiwa kwa saa saba na kurushwa
na Televisheni ya Taifa (TBC) kwa saa moja tu, huku wabunge wa upinzani
wakiondolewa na kuonyeshwa wa CCM pekee.
Alitaka vyombo vya
habari vya elektroniki kuruhusiwa kurekodi shughuli za Bunge na kurusha
maudhui wanayoyataka, badala ya kupewa video na studio ya Bunge ambayo
huondoa michango na hoja za wapinzani.
Mchungaji Msigwa, Masoud
Abdallah, Kamili, Matiko waliungana na Salehe na kusisitiza kuwa nchi
nyingi barani Afrika zinarusha ‘live’ matangazo ya Bunge huku wakihoji
sababu za TBC kurusha moja kwa moja harusi na kushindwa kuonyesha
shughuli za Bunge.
Mbarouk alikwenda mbali akitaka Bunge kuanza
shughuli zake usiku ili kuendana na utetezi wa Waziri wa Habari, Nape
Nnauye kuwa usiku wananchi wengi wanakuwa majumbani mwao hivyo wanapata
nafasi nzuri ya kufuatilia Bunge.
Mbunge wa Jimbo la Tarime Mjini(Chadema),Ester Matiko,anasema;"Juzi Rais John
Magufuli kazindua Daraja la Kigamboni, TBC ilikata matangazo ya Bunge
ili kuonyesha uzinduzi huo. Yaani ya kwenu mnataka yaonyeshwe ila haya
ya Bunge yasionekane. Mnakiuka demokrasia."
Hata hivyo;Hawa Ghasia (Mtwara Vijijini) anasema "Demokrasia
siyo Bunge kuonyeshwa ‘live’. Wakulima na wafugaji hawawezi kuona Bunge
asubuhi ndiyo maana yanarushwa usiku."
Mbunge wa Jimbo la Kigoma Kaskazini(CCM),Peter Serukamba,anaongeza;"Mbona wabunge wa
Chadema wanaonyeshwa katika matangazo ya TBC. Hoja kwamba maagizo ya
Serikali hayatawafikia watendaji si kweli."
Mwanasheria Mkuu wa
Serikali (AG), George Masaju anasema wapinzani hawajiamini na
hawaaminiki huku akiwataka wasome ibara ya 100 ya Katiba.
Anasema;“Bunge
kuonyeshwa au kutoonyeshwa hakuongezi kitu jimboni. Wanaozungumza ni
wabunge siyo televisheni.”
Akihitimisha hoja, Kairuki alipinga
maelezo ya Salehe na kutoa mfano wa nchi ambazo matangazo ya Bunge
hayarushwi moja kwa moja.
Kutokana na mvutano huo Chenge
aliwahoji wabunge wanaoafiki hoja ya Salehe waseme “ndiyooo”, wapinzani
pekee wakasema ndiyoo, aliposema wasioafiki waseme siyo, wabunge wa CCM
kutokana na wingi waliitikia kwa sauti kubwa siyoooo, na Chenge akasema
anadhani wasioafiki wameshinda.
Kufuatia hali hiyo kwa zaidi ya
mara tano,wabunge wa upinzani wameshuhudiwa wakijirekodi
ndani ya ukumbi wa Bunge kwa kutumia simu zao za mkononi, wanapotoka nje
huulizana kama wameshatumia video na sauti hizo katika mitandao ya
kijamii.
Juzi, Mbunge wa Ukonga (Chadema), Mwita Waitara baada
ya kumaliza kuchangia mjadala wa bajeti ya Ofisi ya Rais (Tamisemi na
Utawala Bora) alirusha sauti yake katika mitandao ya kijamii na kusema
hiyo ni moja ya njia ya kuwafanya wananchi wajue kinachoendelea bungeni.
KUONA VIDEO MPYA BOFYA HAPA CHINI