SERIKALI imehakikisha kuendelea kusimamia mazingira kwa kukabiliana na changamoto ya kuzagaa kwa mifuko ya plastiki inayotumika nchini kwa kuhakikisha upatikanaji wa bidhaa hiyo ikiwa imekidhi viwango vinavyokubalika.
Kauli
hiyo imetolewa leo Bungeni mjini Dodoma na Waziri wa Nchi, Ofisi ya
Makamu wa Rais, Mazingira na Muungano January Makamba alipokuwa akitoa
hoja ya wizara yake kuidhinishiwa maombi ya fedha kwa mwaka wa fedha
2016/2017.
Makamba
amesema kuwa sababu kubwa ya kusambaa kwa mifuko ya plastiki inatokana
na mifuko hiyo kutolewa bure na hivyo kuchafua mandhari na kuziba
mifereji sehemu mbalimbali hali inayosababisha athari kubwa katika
mazingira.
“Asilimia
kubwa kwenye mito, maziwa na fukwe za bahari imejaa mifuko ya plastiki,
hali hii ni hari kwa usalama wa mazingira yetu” alisema Makamba.
Akiwasilisha
hotuba yake, Waziri Makamba amesisitiza kuwa mifuko ya plastiki
isiyotakiwa kutumika nchini ni ile yenye unene chini ya maikroni 50
ambayo hairuhusiwi kuzalishwa wala kuingizwa.
Kwa
mujibu wa maelekezo ya bajeti ya mwaka wa fedha 2015/2016, Waziri huyo
amesema kuwa Ofisi ya Makamu wa Rais imekamilisha kanuni mpya ya mifuko
ya plastiki zinazorekebisha viwango vya unene unaoruhusiwa kutoka
Maikroni 30 kwenda Maikroni 50.
Waziri
Makamba amesema kuwa kanuni hizo tayari zimesainiwa kupitia tangazo la
Serikali Na.271 la mwaka 2015 na kutolewa katika Gazeti la Serikali
Julai 17, 2015 na kupewa Na. 29.