MAAZIMIO
YA BARAZA KUU LA UONGOZI LA TAIFA LA CHAMA KATIKA KIKAO CHAKE CHA
TAREHE 2 – 3 APRILI, 2016 KILICHOFANYIKA MAZSONS HOTEL, MJINI ZANZIBAR
BARAZA
Kuu la Uongozi la Taifa la THE CIVIC UNITED FRONT (CUF – Chama Cha
Wananchi) limefanya kikao chake cha kawaida kwa siku mbili, tarehe 2
hadi 3 Aprili, 2016 mjini Zanzibar chini ya Mwenyekiti wa Kamati ya
Uongozi ya Chama, Mheshimiwa Twaha Taslima.
Ajenda
kuu ya kikao hicho ilikuwa ni Hali ya Kisiasa Zanzibar na mwelekeo wa
CUF baada ya kufanyika kile kilichoitwa uchaguzi wa marudio wa tarehe 20
Machi, 2016.
Baada ya kupokea na kujadili kwa kina ajenda hiyo, Baraza Kuu la Uongozi la Taifa limefikia maazimio yafuatayo:
1. Linawapongeza
wananchi wote wa Zanzibar kwa ujasiri, uzalendo na ari kubwa
walioionesha kwa kuitikia kwa kiasi kikubwa wito wa chama chao cha CUF
wa kuwataka wasishiriki katika uhuni na ubakaji wa demokrasia uliopewa
jina la uchaguzi wa marudio wa tarehe 20 Machi, 2016.
Baraza
Kuu la Uongozi limefurahishwa kuona zaidi ya asilimia 80 ya wapiga kura
wa Zanzibar hawakujitokeza kushiriki katika uchaguzi huo haramu na
batili, na hivyo kuudhihirishia ulimwengu kwamba Chama Cha Mapinduzi
(CCM) hakina ridhaa ya wapiga kura hao.
2. Linawapongeza
waliokuwa wagombea wa CUF kwa nafasi zote za Urais, Uwakilishi na
Udiwani kwa kuheshimu maamuzi ya Chama na kutoshiriki uchaguzi haramu na
batili wa marudio licha ya njama nyingi zilizokuwa zikifanywa na Tume
ya Uchaguzi ya Zanzibar chini ya Mwenyekiti wake, Jecha Salim Jecha, za
kulazimisha ushiriki wao. Msimamo wa wagombea hao umewadhihirishia na
kuwathibitishia CCM kwamba tofauti na wao, viongozi wa CUF hawajali
nafasi na vyeo binafsi bali wanachotaka ni kuleta mabadiliko ya kweli
kwa maslahi ya watu wote wa Zanzibar.
3. Linawapongeza
kwa namna ya pekee wagombea Urais, Uwakilishi na Udiwani wa vyama
vyengine vya upinzani ambavyo ni UMD, JAHAZI ASILIA, CHAUMMA, UPDP, DP,
na ACT-WAZALENDO, na vile vinavyoshirikiana kupitia UKAWA ambavyo ni
CHADEMA, NCCR na NLD vilivyoungana na wananchi wa Zanzibar kususia
uchaguzi haramu na batili wa marudio na kusimamia maamuzi halali ya
wapiga kura waliyoyafanya kupitia uchaguzi mkuu halali wa tarehe 25
Oktoba, 2015.
4. Linazishukuru
na kuzipongeza jumuiya na taasisi zote za kitaifa na kimataifa pamoja
na nchi rafiki za Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ambazo zilikataa
kuleta waangalizi wa uchaguzi katika uchaguzi huo haramu na batili na
hivyo kuungana na Wazanzibari katika kutetea maamuzi yao halali
waliyoyafanya katika uchaguzi mkuu halali uliokuwa huru na wa haki wa
tarehe 25 Oktoba, 2015.
5.
Linavishukuru na kuvipongeza vyombo vya habari vya ndani na nje ya nchi
pamoja na waandishi wa habari na wapiga picha kwa jinsi vilivyosaidia
kuonesha ulimwengu uchaguzi mkuu uliokuwa halali, huru na wa haki wa
tarehe 25 Oktoba, 2015 na pia kwa jinsi vilivyoanika uchafuzi wa tarehe
20 Machi, 2016 hasa kule kuonesha vituo vya kupigia kura vikiwa havina
watu na hivyo kuwasaidia Watanzania na ulimwengu kuujua ukweli ambao CCM
na Tume yao ya Uchaguzi walikuwa wakijaribu kuuficha.
6. Linalaani
tabia na mwenendo wa uongo, uzushi, na uvunjwaji wa Katiba, Sheria na
Maadili wa Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar, Jecha Salim
Jecha, dhidi ya matakwa na maamuzi halali ya Wazanzibari waliyoyafanya
katika uchaguzi mkuu huru na wa haki wa tarehe 25 Oktoba, 2015 na
kitendo chake cha kuiingiza Zanzibar katika dimbwi la chuki, uhasama,
uvunjifu wa haki za binadamu na udhalilishaji wa raia kwa sababu tu ya
kukiridhisha chama chake cha CCM ambacho kimekataliwa na Wazanzibari.
Vitendo
vya Jecha Salim Jecha vimeishushia hadhi Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar
na kuichafulia jina Zanzibar na Jamhuri ya Muungano wa Tanzania mbele ya
jumuiya ya kimataifa na kuonekana haiko tofauti na nchi nyengine za
Afrika zisizoheshimu matakwa na maamuzi ya wananchi katika uchaguzi.
7.
Linalaani hatua ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dk.
John Pombe Magufuli kuleta nguvu kubwa ya vikosi vya ulinzi na usalama
kuja kubaka demokrasia Zanzibar.
Baraza
Kuu linalaani vikali nguvu kubwa iliyotumiwa na vyombo vya dola dhidi
ya raia wasio na hatia kwa lengo na madhumuni ya kuwatisha na kuwazuia
wasitumie haki zao za msingi kama ibada kwa kuwalazimisha kutotoka nje
ya nyumba zao kuanzia saa 2 usiku wakati muda huo ni muda wa ibada ya
sala kwa Waislamu ambao ni asilimia 99 ya wananchi wote wa Zanzibar.
Baraza
Kuu pia linalaani mwenendo wa viongozi wa juu wa vyombo vya ulinzi na
usalama wa kutumika waziwazi kisiasa kwa kuegemea upande wa CCM na
kuwakandimiza viongozi na wanachama wa CUF kinyume na maadili ya kazi
zao.
8. Linalaani
vitendo vya Serikali kuunda makundi ya kiharamia ambayo yamekuwa
yakiwahujumu raia wasio na hatia yakitumia silaha za moto na silaha za
kienyeji huku yakitumia gari za Idara Maalum za SMZ.
Baraza
Kuu linalaani Jeshi la Polisi ambalo limekuwa likiyalinda makundi haya
na kutochukua hatua zozote dhidi yao licha ya wananchi wanaohujumiwa
kutoa taarifa kwa jeshi hilo.
Badala yake, katika matukio mengi Polisi imewageuzia kibao wananchi waliohujumiwa kwa kuwakamata na kuwaweka ndani.
Baraza
Kuu linawataka Wakuu wa Jeshi la Polisi kujirudi, kutekeleza majukumu
yao ya kulinda usalama wa raia na mali zao na na kufuata maadili yao na
kuwacha kujifanya ni Idara ya Polisi ya CCM.
9. Haliyatambui
matokeo ya uchaguzi huo haramu na batili, na kwa msingi huo halimtambui
Dk. Ali Mohamed Shein kuwa Rais wa Zanzibar, haliwatambui waliotangazwa
kuwa Wawakilishi na wala haliwatambui waliotangazwa kuwa Madiwani.
Baraza
Kuu linaungana na wananchi wa Zanzibar waliokataa kuwapa uhalali watu
hao na kwa hivyo halitoitambua Serikali, Manispaa na Halmashauri za
Wilaya zitakazoundwa na watu hao.
CUF
haitoshirikiana na Serikali itakayoundwa kwa sababu ni kinyume na
Katiba ya Zanzibar, kinyume na Sheria ya Uchaguzi na haikutokana na
ridhaa ya watu.
Kwa
vyovyote vile, Serikali itakayoundwa haitakidhi matakwa ya Katiba ya
Zanzibar na hivyo CUF haitoshiriki kwenye uvunjaji wa Katiba ambayo
inaeleza kwa uwazi kabisa namna ya kuundwa kwa Serikali ya Umoja wa
Kitaifa Zanzibar.
10.
Linawataka wananchi wote wa Zanzibar kutumia njia za amani, za kikatiba
na kisheria ambazo zimewahi kutumika katika nchi nyingine duniani
kuwakataa watawala waovu na wasio na ridhaa ya watu waliojiweka
madarakani kwa kutumia nguvu na ubakaji wa demokrasia kwa kutoipa
ushirikiano Serikali itakayoundwa na watawala hao.
11.
Linaendelea kuutambua uchaguzi mkuu uliokuwa halali, huru, wa haki na
uliofanyika katika hali ya amani na utulivu wa tarehe 25 Oktoba, 2015 na
pia linayatambua matokeo yake ambayo yalionesha wazi kwamba chaguo la
Wazanzibari ni CUF na Maalim Seif Sharif Hamad kuiongoza Serikali ya
Umoja wa Kitaifa Zanzibar.
Kitendo
cha zaidi ya asilimia 80 ya Wazanzibari kususia uchaguzi haramu na
batili wa tarehe 20 Machi, 2016 kimezidi kuyapa nguvu maamuzi yao ya
tarehe 25 Oktoba, 2015 mbele ya macho ya Watanzania na dunia.
12.
Linaendelea kuwataka Wazanzibari kuwa watulivu na kulinda amani iliyopo
na linawahakikishia kwamba CUF inaendelea na juhudi zake za kutafuta
haki yao na kusimamia maamuzi yao waliyoyafanya tarehe 25 Oktoba, 2015
kwa njia za amani na za kidemokrasia. Njia hizo za amani zimefanikiwa na
kuungwa mkono na jumuiya ya kimataifa ambayo imeanza kuchukua hatua
dhidi ya ubakwaji wa demokrasia uliofanyika.
13.
Linazishukuru na kuzipongeza nchi washirika wa maendeleo kwa kuchukua
maamuzi ya kuzifutia misaada Serikali za kidikteta za CCM ambazo
zimebaka demokrasia na kukanyaga haki za wananchi wa Zanzibar.
Baraza
Kuu linatoa wito kwa nchi hizo washirika wa maendeleo na jumuiya za
kimataifa kuchukua hatua zaidi dhidi ya Serikali za CCM na madikteta
wake walioshiriki katika ubakaji wa demokrasia Zanzibar zikiwemo hatua
makhsusi dhidi ya watu makhsusi waliohusika na ubakaji huo wa demokrasia
na uvunjaji wa haki za binadamu katika kipindi hiki.
MWISHO,
Baraza Kuu la Uongozi la Taifa linawahakikishia wanachama wake wote na
Watanzania kwa ujumla kwamba chama chao kiko imara na hakitoyumba wala
kuyumbishwa katika kutetea na kupigania haki zao hadi tutakapofanikisha
ujenzi wa taifa imara linalosimamia na kuheshimu utawala wa sheria, haki
za binadamu, demokrasia na utu wa watu wote.
Baraza
Kuu linawataka viongozi wa Chama wa ngazi zote watekeleze majukumu yao
ya kichama katika nafasi zao na pia Wabunge na Wawakilishi waliopewa
ridhaa na Wazanzibari tarehe 25 Oktoba, 2015 kuwatumikia wananchi wote
katika kutatua matatizo yao kadiri hali na uwezo wao unavyoruhusu.
Mbali
na maazimio haya, Maalim Seif Sharif Hamad atazungumza na wananchi
katika siku chache zijazo ili kuwaeleza kwa kina mwelekeo wa hali ya
kisiasa ya Zanzibar na hatua zinazochukuliwa na CUF kuhakikisha maamuzi
halali ya kidemokrasia ya Wazanzibari waliyoyafanya tarehe 25 Oktoba,
2015 yanaheshimiwa.
HAKI SAWA KWA WOTE
Limetolewa na:
BARAZA KUU LA UONGOZI LA TAIFA
THE CIVIC UNITEDN FRONT (CUF – Chama Cha Wananchi)
ZANZIBAR
3 APRILI, 2016
KUONA VIDEO MPYA BOFYA HAPA CHINI