SAKATA la yatapojengwa Makao Makuu ya
Halmashauri ya Msalala,wilayani Kahama,limeingia sura mpya baada ya Umoja wa
Wazee wa wilaya ya Kahama(UWAKA)kujitokeza na kuishauri Serikali kuheshimu
maamuzi ya Baraza la Madiwani.
Baraza hilo lilifanya kikao hicho mjini
Kahama,na kuunga maadhimio ya Baraza la Madiwani ya kutaka Makao Makuu hayo
kujengwa Kata ya Mega,badala ya Busangi kama yalivyopitishwa awali,na kudumu
kwa miaka minne tangu Halmashauri hiyo ilipogawanywa kutoka Halmashauri ya
wilaya ya Kahama.
Katibu wa Uwaka,Paul Ntelya,alisema wazee
wanaafikiana na Baraza la Madiwani makao makuu hayo yawe Kata ya Mega,kutokana
na mchanganuo wa maamuzi yao kuzingatia ukubwa wa eneo ambalo wamedhamiria
kuligawa kwa lengo la kusogeza huduma kwa wananchi.
Awali Mwenyekiti wa Kamati ya Elimu,Afya na
Maji;Dkt.Gerald Mwanzia,aliyemwakilisha Mwenyekiti wa Halmashauri ya
Msalala,aliwaeleza wazee hao kuwa msingi wa maamuzi yao ulikuwa sambamba na
kuomba uwepo wa Mamlaka ya Mji mdogo wa Isaka ,hatua itakayosaidia kusukuma
maendeleo ya Halmashauri yao.
“Tumeangalia maendeleo zaidi ya wilaya ya
Kahama,hivyo kama Makao Makuu yatakuwa Mega,huku ikipatikana Mamlaka ya Mji
Mdogo wa Isaka itakayokuwa na Kata tano,itapunguza ukubwa wa Halmashauri hivyo
kusogeza huduma kwa wananchi inavyostahili,”alisema Dkt.Mwanzia ambaye pia ni
Diwani wa Kata ya Isaka.
Katibu wa Uwaka,Ntelya alidai mgogoro wa
makao Makuu unasababishwa na maslahi binafsi ya baadhi ya viongozi,wakiwemo
wanasiasa na kudai wanatoa ushauri huo kama ulivyo wajibu wa umoja wao ili
kuona suala hilo linafikia ukomo kwa maendeleo ya wilaya ya Kahama.
Nae Mjumbe wa Uwaka,Khalfani Mandwa,alisema suala
hilo lisitumike kama mtaji wa kisiasa kwa wawakilishi hao wa wananchi,hvyo
wasiyumbishwe tena bali wasimamie maamuzi yao hayo ambayo yamelenga kuhakikisha
yanasogeza maendeleo kwa wananchi,na pindi akitokea miongoni mwao kubadilika
hawana budi kumweka hadharani kwa wananchi.
Mvutano huo umedumu kwa miaka minne
na tayari kwa mujibu wa Mkurugenzi wa Halmashauri ya Msalala Patrick Karangwa
serikali ilitoa shilingi milioni 500 kwa ajili ya ujenzi wa makao hayo huko
Busangi lakini mvutano huo umekwamisha ujenzi huo,wa Halmashauri hiyo
iliyoanzishwa na ile ya Ushetu kutoka Halmashauri mfu ya wilaya ya Kahama.