MSICHANA Asha Sudi (17), mkazi wa
Tabata Kisiwani,amejikuta akijifungulia mtoto chooni baada ya
muuguzi mmoja wa Hospitali ya Amana jijini Dar es Salaam kumtaka aende kuoga na
kubadilisha nguo bila ya kujali hali yake ya uchungu uliokuwa ukimkabili.
Msichana huyo, alikutwa na tukio
hilo juzi wakati akisubiri kujifungua,baada ya kufika hospitalini hapo majira
ya saa 4:00 asubuhi akiwa anaumwa na uchungu, na kutakiwa na wauguzi wa mapokezi
kuketi katika benchi.
Alisema wakati akiwa ameketi katika benchi
hilo alifika Nesi na kumuamuru aende kuoga na kubadilisha nguo chooni pasipo
kujua alitekeleza agizo hilo,na wakati akiwa chooni anajiandaa kuoga, uchungu
ulikata ghafla na baada ya dakika chache aliona kitu kinaning’inia sehemu za
siri kisha kikadondoka chini.
Alisema baada ya kuona hivyo,
alianza kupiga kelele kwa kuiita “nesi, nesi” na ndipo alipopita wa kwanza
ambaye hata hivyo hakumshughulikia na badala yake akaendelea na kazi zake,
lakini baadaye akaenda daktari ambaye hakumtambua kwa jina, akamsaidia.
“Nilianza kutapatapa huku nikiita na kupiga mayowe ndipo alifika daktari
akamuokota mtoto ambaye alikuwa ameanguka chini karibu na tundu la choo,”alisema.
Baadhi ya wauguzi walitoa ushuhuda
wa tukio hilo, wakiwamo daktari aliyemuokoa mama huyo na mwanaye chooni, lakini
hawakutaka majina yao yatajwe
“Nilikuwa
wodini. Wakati napita nikasikia mtu anapiga kelele chooni akiita ‘nesi, nesi,
mwanangu jamani’. Nilishtuka, ikabidi niende kuona ndipo nikamkuta huyo binti
akiwa amesimama na kondo likiwa limening’inia na kitoto kichanga kimeanguka
chini,” alisema.
Alieleza kuwa alikiokota kichanga
hicho na mama yake kisha kuwapa huduma ya kumsafisha mtoto.
Muuguzi mwingine ambaye alikuwa zamu
mchana, alisema alipopita kumuangalia mtoto huyo, alikuta akiwa na uvimbe
kwenye paji la uso.
“Nikamuuliza
mama wa mtoto ndipo akanisimulia. Kwanza nikashangaa huyu nesi ilikuwaje
akamruhusu mama ambaye anataka kujifungua kwenda chooni?” alihoji.
Mkuu wa Idara ya Wazazi, Grace
Massawe alisema wamelichukua suala hilo na kwamba watalishughulikia kikamilifu,
lakini akawataka wazazi na ndugu wa mama huyo kuwa watulivu na kuwasamehe
waliofanya tukio hilo.
Mkuu wa Idara ya Mama na Mtoto wa
hospitali hiyo, Francis Kioweli alisema mtoto huyo hajapata athari ya kiafya na
kwamba endapo kutatokea tatizo lolote, basi wazazi hao wasisite kwenda
hospitali kwa uangalizi zaidi.