MGOGORO wa sehemu
itakayojengwa Ofisi za Makao Makuu ya Halmashauri ya Msalala,wilayani Kahama,mkoani
Shinyanga,umeanza upya kufuatia msimamo wa Serikali kuagiza yajengwe Busangi
huku Madiwani wengi wa Halmashauri hiyo wakitaka yajengwe katika Kata ya Mega.
Hayo yalibainika jana
katika Kikao maalumu cha Madiwani wa Halmashauri ya Msalala na Mkuu wa Mkoa wa
Shinyanga,Ally Rufunga,alipowasilisha tamko la Serikali kupitia ofisi ya
Rais,Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa “TAMISEMI”.
Rufunga alisema Serikali
imeyakataa maombi ya Madiwani hao,kutaka Makao Makuu hayo yahamishwe Kata ya
Busangi na kupelekwa Kata ya Mega,kama suluhisho la mvutano wa muda mrefu wa
Makao Makuu hayo kujengwa Busangi ama Segese.
Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga
alisema Madiwani kupitia vikao vyao halali walipendekeza Makao Makuu ya
Halmashauri hiyo yawe katika Kata ya Busangi na baadae walipendekeza kubadili
Makao Makuu hayo yahamishiwe katika Kata ya Segese.
Mkuu wa Mkoa huyo
alifafanua kuwa hali hiyo ilileta mvutano kati ya madiwani hao hadi kuanza
mchakato mpya wa makao makuu hayo kuhamishiwa Mega na kabla ya hatua yoyote
kuchukuliwa Serikali ilitoa maelekezo ya kukataliwa kwa maombi ya kwanza ya
kuhamishia Segese.
Kufuatia kwa kauli hiyo
Rufunga aliagiza kuanza kwa ujenzi kwa Makao Makuu hayo katika Kata ya Busangi,na
yule ambaye ataona hajaridhishwa na
uamuzi huo wa Serikali,wakiwemo Madiwani wanatakiwa kujihudhuru nyadhifa zao
ili waachie watu wengine kuongoza.
MWENYEKITI wa Halmashauri Msalala,Mibako Mabubu. |
Mabubu alisema hata
ushauri wa kutafuta sehemu nyingine nje ya Busangi na Segese,na kupendekezwa
Mega ulitolewa na Mkuu wa Mkoa,Rufunga na Madiwani wote kuafiki lakini kiongozi
huyo alienda TAMISEMI kuzuia azimio hilo halali la Madiwani.
Alisema Madiwani
walikubaliana kupeleka Makao hayo Mega,pia Kamati ya Ushauri ya Maendeleo ya
Wilaya “DCC”nayo iliafiki na kilichokuwa kikisubiriwa ni kikao cha Kamati ya
Ushauri ya Maendeleo ya Mkoa “RCC”kupitisha
na kupeleka TAMISEMI na kwamba wameshangazwa na kauli hiyo ambayo hawako tayari
kuikubali.
Mgogoro wa sehemu ya kujengwa
Makao Makuu ya Halmashauri ya Msalala ulianza mwaka 2013,bila kufikia suluhisho
la kudumu huku baadhi ya viongozi na wananchi wakidaiwa kuendeleza marumbano
kwa njia za siri hali inayodumaza maendeleo ya Halmashauri hiyo.