PAMOJA na kwamba Chama cha Wananchi
(CUF),kuiandikia barua Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC),ikisema imejitoa katika
uchaguzi wa Mbunge Jimbo la Kijitoupele,Zanzibar,NEC imedai haitambui
maamuzi hayo licha kwamba imepokea barua
rasmi toka kwa uongozi wa Chama hicho.
Kwa mujibu wa Mkurugenzi wa uchaguzi
wa Tume ya Taifa,Kailima Ramadhani,alisema Tume imefikia maamuzi hayo kutokana
na chama hicho cha CUF kuchelewa kuwasilisha barua hiyo,ilhali maandalizi ya
Uchaguzi huo yakiwa yamekamilika na wananchi wakisubiri kupiga kura kesho.
Kailima alifafanua kuwa,wamechelewesha
barua yao wakati tayari wameishagharamia kuchapisha karatasi za kupigia kura na
kuwasili hapa nchini tayari kwa uchaguzi huo,na kusisitiza kwamba zitaendelea
kuwa na picha za Wagombea wa CUF hata kama wamejitoa katika uchaguzi huo.
Awali,wajumbe wa Tume ya Taifa ya
uchaguzi wakiongozwa na Makamu Mwenyekiti wa Tume Jaji mstaafu Hamid
Mahamood Hamid walitembelea katika vituo mbalimbali vya kupigia kura
katika Jimbo la Kijitoupele ili kujiridhisha na maandalizi ya uchaguzi huo
kabla ya uchaguzi kufanyika jumapili.
Tume ilibaini kuwepo kwa baadhi ya
kasoro ndogondogo katika baadhi ya vituo vya kupigia kura ikiwa ni pamoja na
kubanduliwa kwa karatasi zenye majina ya wapiga kura,mfano katika kituo cha
Skuli ya sekondari Kinuni.
Jimbo la Kijitoupele lina jumla ya
Wapiga kura wapatao 17,274 na vituo vipatavyo 53 vitatumiwa na wapiga kura ili
kumchagua mbunge wa Jimbo la Kijitoupele siku ya Jumapili.
Uchaguzi katika jimbo la Kijitoupele
uliahirishwa mwaka jana kutokana na hitilafu ndogondogo zilizojitokeza katika
karatasi za kupigia kura,kabla ya kufutwa kwa matokeo ya Uchaguzi mkuu wa
Zanzibar uliofanyika Oktoba 25,2015.
Sambamba na Uchaguzi wa ubunge
katika Jimbo la Kijitoupele, marudio ya uchaguzi mkuu wa Zanzibar Oktoba
25,2015 ambayo matokeo yake yalifutwa utafanyika Jumapili hiyo pia.
KUONA VIDEO MPYA BOFYA HAPA CHINI