RAIS wa Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli, ametoa wito kwa kila mtanzania
kuchapa kazi kwa juhudi,hatua itakalolosaidia kuondokana na utegemezi wa
misaada ya wafadhili,inayoambatana na masharti.
Akiongea na umati mkubwa
wa watu uliojitokeza katika uwanja wa shule ya sekondari Chato, iliyo kijiji
cha Mlimani, Wilaya ya Chato Mkoani Geita,alisema jukumu kubwa lililo mbele ya
watanzania kwa sasa, ni kushikamana na kujisimamia katika maendeleo ili kila
mmoja ahakikishe anaongeza uzalishaji na utendaji kazi mahali pake pa kazi.
Rais Magufuli alisisitiza
kwamba ni wakati muafaka kwa kila Mtanzania katika sekta yake
ama;mkulima,mfanyabiashara,mfanyakazi,mvuvi hata mfugaji ni budi awajibike kwa
nguvu kwa lengo ya kuboresha mapato yake na Taifa,hatua itakayosaidia kuivusha
nchi kwa kuiletea maendeleo stahiki.
Aidha, Rais Magufuli aliahidi
kuendelea kuwachukulia hatua watumishi
wa umma wanaolisababishia taifa upotevu mkubwa wa fedha, kwa kutumia kauli mbiu
yake ya "Kutumbua Majipu" hadi
tatizo hilo litakapokomeshwa,na kurejesha sambamba na kudhibiti nidhamu
serikalini.
Dkt. Magufuli pia alikumbusha
viongozi wote wakiwemo Wakuu wa Mikoa, Wakuu wa Wilaya, Makatibu Tawala na
Wakurugenzi, kutekeleza wajibu wao ipasavyo na ameweka bayana kuwa mahali
popote ambapo hapatakuwa na ufanisi, kiongozi husika atakuwa amedhihirisha kuwa
hatoshi kuendelea na wadhifa aliopewa.
Rais Magufuli aliwapongeza
walimu kote nchini kwa kufanya kazi nzuri ya kufundisha, licha ya changamoto ya
ongezeko kubwa la wanafunzi waliojiunga darasa la kwanza mwaka huu, lakini
ametaka Wazazi na kamati za shule kushirikiana na walimu kuwasimamia wanafunzi
ili waweze kufanya vizuri katika masomo yao.
"Niziombe
kamati za shule zote Tanzania nzima, kama haziwezi kusimamia nidhamu ya
wanafunzi shuleni, zile kamati za shule zijiuzulu. Lakini pia kama wewe ni
Mwalimu Mkuu, shule yako kila siku inatoa divisheni ziro nyingi kila mwaka,
sioni sababu ya wewe kuendelea kuwa Mwalimu Mkuu" Alisisitiza Dkt. Magufuli.
Kuhusu tatizo la
wafanyakazi hewa, Rais Magufuli amesema uhakiki mdogo uliofanywa hivi karibuni,
umebaini wafanyakazi hewa 1,680 waliokuwa wakilipwa shilingi bilioni 1 na
milioni 800, na kwamba ni matarajio kuwa uhakiki unaofanywa nchi nzima
utaisaidia serikali kubaini wafanyakazi hewa wengi zaidi na kunusuru fedha
nyingi zaidi za watanzania.
Alitoa mfano wa mfanyakazi
mmoja wa Mamlaka ya Mapato Nchini (TRA) ambaye alikuwa akilipwa mishahara ya
watu 17, na kueleza kuwa mfanyakazi huyo atafikishwa mahakamani.
Pia Rais Magufuli alisema
serikali yake imejiandaa kuboresha maslahi ya wafanyakazi kwa kupunguza kodi
kutoka asilimia 11 ya sasa hadi asilimia 10 au 9 kuanzia bajeti ijayo, lakini
amesema kwa wale wanaolipwa mishahara mikubwa ambayo inafikia hadi shilingi
milioni 40, itapunguzwa na kuweka kima cha juu cha mshahara usiozidi shilingi
milioni 15.
Rais Dkt.Magufuli amefanya
ziara yake ya kwanza mkoani Geita kwa kufika nyumbani kwake katika kijiji cha
Mlimani, kwa mara tangu achaguliwe kuwa Rais,ambapo alalakiwa na
umati mkubwa wa wananchi ambao walijitokeza pia kwa wingi katika mkutano wa
hadhara.
KUONA VIDEO MPYA BOFYA HAPA CHINI