*Wananchi hawahitaji mgawanyiko wa
uongozi na malumbano wanataka maendeleo.
*Msaidieni Rais tushinde Vita ya
Rasilimali za nchi
HIVI karibuni Rais wa Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt John Pombe Magufuli alipokea ripoti ya Kamati ya
kwanza na ya pili ya uchunguzi wa makontena 277 ya mchanga wa madini
(makinikia) yaliyokuwa njiani kusafirishwa nje ya nchi na uchunguzi ulifanyika
na kulibaini
ndani ya mchanga huo kuna dhahabu na madini mengine kwa asilimia
kubwa.
Aidha, Mhe Rais amechukua hatua
mbalimbali kulingana na ushauri wa kamati husika, pamoja na maamuzi yake kama
Rais. Kutokana na sakata hilo.
Idara ya Habari-MAELEZO imepata fursa
ya kufanya mahojiano na Waziri Mkuu na Makamu wa Kwanza wa Rais wa Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania Mstaafu Mheshimiwa, Jaji Joseph Sinde Warioba katika ofisi
zake zilizopo Osterbay Jijini Dar-es-salaam.
SWALI: Ninanukuu maneno ya Baba wa Tafa, Hayati Mwl
Julius Kambarage Nyerere kuhusu raslimali za nchi na hususan madini alisema:
“Madini yetu tuliyonayo ni vema kuyaacha mpaka Watanzania watakapokuwa na
ufahamu wa kutosha wataamua kuyachimba” mwisho wa kunukuu nini maana yake?
JIBU: Mara baada ya
Uhuru wa Tanganyika mwaka 1961 Hayati, Mwalimu Julius Kambarage Nyerere
alipokea nchi kama Waziri Mkuu wa kwanza wa Tanganyika huru akiwa hana
wataalamu zaidi ya madaktari 2 na yeye mwenyewe ambaye alikuwa msomi kutoka
chuo Kikuu cha Edinburg Uingereza. Kwa hali hiyo, Mwalimu alikuwa sahihi
usingeweza kuruhusu rasilimali za nchi mfano madini kuchimbwa na wageni kutoka
nje maana yake Watanganyika wangekuwa watazamaji tu bila kufaidika na lolote.
Mwalimu alihakikisha anawekeza katika
elimu ambayo ilikuwa bure kuanzia msingi hadi chuo kikuu. Na elimu ndio msingi
wa kuondoa Ujinga, Umasikini na Maradhi. Alitambua Watanganyika wakielimika na
kupata utaalamu wa madini ikiwa ni pamoja na uchimbaji watakuja kuyachimba na
kufaidika.
SWALI:Tanzania ni kati ya nchi zilizobarikiwa kuwa na
raslimali nyingi za kila aina kuanzia madini, gesi, wanyamapori na hifadhi,
misitu, milima, maporomoko ya maji, mabonde maziwa makubwa kwa madogo, bahari
ya hindi na raslimali za mazao ya uvuvi, nchi yenye ardhi ya kutosha watanzania
wenye uwezo wa kufanyakazi kwa ufanisi. Unadhani nini tatizo letu na nini cha
kufanya?
JIBU: Sioni kama
kuna tatizo la msingi, lakini ni suala la uelewa mara nyingi kuna watu ambao
huamini viongozi wao kwa kila kitu wanachosema. Lazima wananchi wawe makini kwa
sababu tatizo la watanzania ni maendeleo kila mwananchi ana kiu ya kutaka
tufikie mahala pazuri kama Taifa na mimi nakubaliana nao kabisa.
Tuna rasilimali nyingi, ambazo
kimsingi tukiweza kuzishughulikia kwa makini kama lilivyoshughulikiwa suala la
mchanga wa madini tutakuwa mbali sana kiuchumi.
Mosi, tuangalie rasilimali ya madini
kwa mapana yake na kushughulikia wawekezaji wa ndani na wale wa nje, Barick na
Acaccia ni sehemu ndogo sana ya madini, tuangalie wachimbaji wa ndani mfano
Tanzanite ni aibu madini yanachimbwa Manyara biashara hii inatokaje Mererani na
kufanyika Nairobi na New Delhi tujiulize kwa nini sio Arusha na Dar-Es-Salam.
Pili, upande wa rasilimali za maziwa
makubwa tuliyonayo Victoria, Tanganyika na Nyasa, Bahari ya Hindi kuanzia Moa
mpaka Tanga kwa kiasi gani tumeweza kutumia rasilimali za bahari maharamia
wanakuja na meli zao wanavuna tu na kuwatajirisha watu wengine. Mfano ziwa
Victoria linategemewa na wananchi wengi na sasa samaki hamna wamekwisha kwa
sababu hatusimamii rasilimali zetu ipasavyo. Maana suala sio kuvuna tu
tunalindaje hizi rasilimali zetu ili ziwepo leo kesho na vizazi vijavyo.
Tatu, Maliasili zetu za wanayamapori,
mbuga za wanyama, vitalu vya utalii unampaje mfanyabiashara kibali cha kuwinda
miaka 99 yaani atumie yeye, wanawe na wajukuu zake, watanzania watatumia lini,
haya ni masuala ya msingi kabisa ya kuangalia upya.
Nne, Ardhi Mwalimu alisema ili
tuendelee tunahitaji vitu vine Watu, Ardhi Siasa Safi na Uongozi Bora. Mwalimu
Nyerere aliona ardhi ndio kilakitu hivyo vyote tulivyovitaja vipo ardhini
pamoja na sisi wanadamu tunaitegemea kwa kila kitu. Maeneo mengi yaliyotumiwa
na watu kwa shughuli za ufugaji aidha , yana matumizi mengine kama nyumba,
kilimo cha mashamba makubwa, na idadi ya watu inaongezeka ardhi ni ileile hii
imesababisha migogoro ya watumiaji wa asili wa maeneo hayo na wenye matumizi
mengine tunatatuaje changamoto hii.
SWALI: Kwa kuwa umebobea katika masuala ya mikataba
na sheria, ushauri gani unautoa katika masuala yote ya raslimali za Tanzania?
Nani anatakiwa kusimamia raslimali hizi kwa ufanisi?
JIBU: Hii sio
suala la mjua sheria au asiyejua, Mwanasheria lazima anazijua sheria ndio maana
amepewa dhamana. Linalojitokeza ni ukosefu wa maadili ya uongozi, imani, utiii,
uwazi na kutopenda nchi yako na Watanzania ambao wamekupa dhamana ya kusimamia
jambo.
Ndio maana Mwalimu Nyerere aliweka
miiko ya uongozi, maadili ya uongozi kwenye Azimio la Arusha. Kila mwananchi
alikuwa anaweza kujua kiongozi huyu muadilifu au sio muadilifu na anachukuliwa
hatua kabla mambo hayajaharibika.
Lakini sio vema kumhukumu mtu kwa
jambo lolote lile, ni vema busara itumike kujua kilichotokea mfano hili suala
la mchanga wa madini ya makinikia.
Jambo la msingi ni kutafuta suluhu
itakayotupeleka mbele, tuone sera zetu zikoje na zinatusaidiaje kulinda
rasilimali za Taifa, tunarekebisha vipi kuondoa tatizo, sheria na utendaji kwa
ujumla. Naomba watanzania tutoe maoni na mawazo yatakayoboresha sera, sheria na
utendaji au usimamizi wa rasilimali husika. Tunaweza kurudisha miiko na maadili
ya uongozi katika kusimamia rasilimali za nchi, kila Mtanzania ajue sio mali
yake ni ya Watanzania wote lazima aitunze vinginevyo atahukumiwa kwa hilo.
SWALI: Ni ukweli usiopingika kuwa kosa limeshafanyika
kwa hili tuliloliona la mchanga wenye madini ya dhahabu, ambapo mhusika ambaye
ni mmiliki wa Kampuni inayobeba mchanga huo tangu 1998 hadi 2017 amewasili
nchini kuonana na viongozi wakuu wa serikali, nini maoni yako kuhusu hili?
JIBU: Sisi
hatukushughulika na uchimbaji wa madini, lakini utafiti tulifanya na kujua
madini yapo na kuna maeneo mengi ambayo tumeweza kufanya vizuri tunapata
mapato, lakini hatukupata mapato yote.
Lakini hili la mchanga sitaki
kulizungumzia sana nadhani watu wanalichukulia kwa mihemko sioni faida
kuzungumzia matukio badala ya kuona tafsiri nzima nini cha kufanya.
Ninachokiona na cha muhimu sana,
Watanzania wamepata faida kwa mara ya kwanza tumeweza kujua mikataba ya madini
ikipitiwa na Kamati zote mbili zimetueleza maeneo yote ya mikataba waliyopitia
na kuja na mapendekezo. Tumetambua serikali ilikuwa na hisa au la mrahaba
asilimia ngapi, kodi kiasi gani, na mambo kama hayo.
Naomba jambo hili lisibague, tunasema
hatupati mapato ya kutosha ni lazima tujue kwa wachimbaji wa nje na wa ndani
mfano nani anajua wachimbaji wadogo wadogo wamechimba madini kiasi gani tangu
1998 hadi 2017 na kodi kiasi gani imeimngia. Tumepata nafasi sasa ya kuangalia
sera za kulinda rasilimali ya madini na nyingine zote katika nchi, kama
maliasili ya bahari tunaitumiaje, gesi, makaa ya mawe, chuma, wanyama pori na
mambo kama hayo.
Hii imetufungua macho sera ya aina
gani sheria za aina gani, jinsi gani ya kutunza na kutumia rasilimali hizi
tulizopewa na mungu.
SWALI: Kwa kuwa wananchi tulio wengi tunaenda kwa
mihemko bila kupambanua hoja husika na kutoa mapendekezo au maoni yatakayo
isaidia serikali kuboresha sera sheria na utendaji wa rasilimali zetu unadhani
tatizo ni nini?
JIBU: Hatujaona
uongozi wa Kitaifa katika hili suala la mchanga wa makinikia ninachokiona mimi
ni uongozi wa chama na siasa nyingi, sio sahihi kabisa wanafanya makosa hili ni
suala la rasilimali za nchi ni la kila Mtanzania.
Viongozi hawawatendei haki wananchi
wanaowakilisha, wanakuwa na mihemko wanasema kamata, shitaki, wafunge. masuala
ya kitaifa hayaendi hivyo sisi sio Polisi wala Mahakama waachieni wenye kazi
yao.
Uongozi wa kulalamika hautusaidii,
wananchi wanataka kuona rasilimali zetu zinanufaisha na kuboresha huduma za
jamii ambazo wanalalamika kila leo hakuna dawa, elimu isiyowajenga vijana na
mambo kama hayo.
SWALI: Mhe. Kutokana na sakata la mchanga wa
dhahabu uliokuwa unasafirishwa nje ya nchi na matokeo yake watanzania
tunajifunza nini kwa maoni yako?
JIBU: Kabla ya
tuona funzo tulilopata nadhani ni vema nikazungumzia jambo hili, nimeona
mjadala katika mitandao ya kijamii ambayo inafanywa kwa mihemko. Ukiangalia
vyombo vya habari au viongozi tumejikita katika majina ya watu, nilikuwa
nnaangalia Bunge wote wanakwenda kwa wale waliotajwa unakuta kuna wanaochangia
na wanaolaumu ama unsahangilia au unalalamika kuhusu watu.
Kubwa ni utaratibu tulionao
haitasaidia kulalamika juu ya watu waliofanya kazi huko nyuma, tunaweza
kuwauliza wahusika nini kilitokea mpaka kufanya hivyo, lakini hilo sio kubwa,
muhimu ni kutafuta ufumbuzi.
Mjadala huu umenikumbusha Awamu ya
kwanza ya Mwalimu Nyerere viongozi wote na wananchi walikuwa wanalalamika kila
kitu wanachokikosa ni kwa sababu ya wakoloni. Mwalimu akasema namnukuu: “Ni
kweli wakoloni wametuleta matatizo mengi sana lakini haitoshi kulaumu wakoloni
bila kuondoa mateso ya wananchi”. Mwalimu akaja na Waraka ambao ulikuwa unaitwa
“Act dont Argue” nadhani bado upo.
Waziri wa Katiba na Sheria Profesa
Palamagamba Kabudi nanukuu amesema. “Napenda kupata maoni tufanye nini kuhusu
suala hili la mchanga wa dhahabu (makinikia).” Namuunga mkono, sasa tumepata
nafasi ya kutoa maoni, mawazo ambayo ni muhimu sana maoni ya wadau katika
uundaji wa sera na sheria
Sasa hivi siamini kama hatuna
utaalamu, nina hakika tunao wa kutosha tatizo ni maadili na hilo lazima
kutafuta ufumbuzi wake, pia tuunge mkono serikali inachofanya kupambana na
rushwa na ufisadi.
“Lakini tusijidanganye bishara ya
madini, mafuta ina changamoto kubwa sana duniani hususan Afrika, maana
unapambana na watu wenye fedha biashara hii popote utakapo kwenda, ambapo
uchumi unategemea mafuta na madini utaona jinsi wakubwa wanavyooneemeka na
rasilimali hizo na kuwaaacha wananchi wakiwa masikini mfano mzuri Nigeria”.
Pamoja na kuangalia maadili na nidhamu
lazima kuwe na uwazi katika mikataba ni muhimu sana.
SWALI: Una maoni na mapendekezo yako kwa viongozi
wote na Mhe Rais katika kumuunga mkono?
JIBU:Kwanza
naliona hili la malumbano yatatugawa, waache tofauti zao hii lawama ya madini
ingekuwa ni mwanzo kwa kuleta mawazo na maoni ya kutengeneza nchi yetu katika
kulinda na kuzitumia rasilimali zote kwa maendeleo ya taifa letu.
Viongozi msaidieni Rais
kulishughulikia kwa pamoja hili si jambo la chama wala Taasisi. Hakuna haja ya
kupeana lawama ukishasema tumekosea unatakiwa ueleze tufanye nini, sio kusema
serikali ichukue hatua kwani serikali ni nani si mimi na wewe sasa kwa nini
hutaki wewe kulitolea maoni?
Tujiamini nimeona katika malumbano
hayo, wengine wanaonekana kama hatujiami kama tukifanya hivi tunaweza
kushitakiwa, mabadiliko yoyote yana machungu yake. Tusije tukapoteza imani
tuliyonayo maana tunaweza tukapoteza mapato yetu lakini ni lazima tufanye kwa
kujenga afya ya rasilimali zetu.
Rais amekutana na mmiliki wa Barick na
kila upande una msimamo wake, tuiachie serikali na nina imani kabisa serikali
itafanikiwa. Kinachonishangaza ni mazungumzo ya baadhi ya viongozi kuwa
serikali ihakikishe tunapata hizo fedha walizo taja kwenye taarifa.
Nadhani hii sio sahihi, tuna imani na
Viongozi wet wakuu haswa Rais, lolote litakaloafikiwa tulipokee na kulikubali
tusije kuanza kulumbana ripoti imesema trilioni 108 ziko wapi? Pia nilisemee
hili la dalili za kupoteza imani, eti tukifanya hivyo tutashitakiwa, sababu ya
mikataba na wawekezaji hawatakuja mimi naamini watakuja tu rasilimali zipo
kwetu hawana jinsi.
SWALI: Msaada wako binafsi kwa Rais au maoni yako kwa
Rais
JIBU: Sisi tupo,
Uongozi ni suala la kupeana vijiti mimi natoka Mara nimepitia utamaduni wa
kabila langu kwa utamaduni wetu unafika mahali unangatuka watu wanadhani
kungatuka ni kustaafu hapana sio sahihi. Ukitoka jandoni mzee wako lazima
angatuke maana umekuwa sehemu ya jeshi la kabila na yeyote ambaye kijana wake
yuko kwenye jeshi yeye anatoka.
Wazee hawaingii katika mambo ya vijana
na sisi tupo lakini hatutaki kuingilia utendaji wao kama sisi tulivyoachiwa
kuendesha nchi, ila Rais akituhitaji tupo tayari kwa ajili ya ushauri anaweza
kuukubali au kuukataa. Nataka nimhakikishie kwa hili tupo pamoja na tutatoa
maoni ya kurutubisha Sera, Sheria na Utendaji katika rasilimali za nchi hii.