WAKULIMA Mkoani Shinyanga,wameshauriwa
kulima zao la Alizeti,kutokana na kuwa na fursa kubwa ya kukuza uchumi wa mkoa
kufuatia
uwepo wa Mwekezaji anayezalisha mafuta huku akikabiliwa na changamoto
ya upatikanaji wa malighafi ya bidhaa hiyo.
Sambamba na uwepo wa Mwekezaji,ambaye
ufanisi wake umekuwa mdogo kutokana na ukosefu wa malighafi ya kutosha,pia
wakulima wanaweza kumudu kumiliki mitambo yenye gharama nafuu ya kukamulia
mafuta,hivyo kujiongezea kipato.
Mwenyekiti wa Kanda ya Ziwa wa Umoja
wa Wazalishaji wa Mbegu za Mafuta ( TEHOSA),Paul Ntelya, alitoa ushauri
huo,huku akisisitiza zao hilo linaweza kuwa mkombozi wa Mkoa kumudu kuanzisha viwanda
vidogovidogo vya utengenezaji wa mafuta kwa wajasiriamali.
Ntelya alisema pindi wakulima wakilima
zao hilo ana imani uchumi wao utakuwa kwa kasi,kutokana na zao hilo mafuta yake
kupendeka kwa kiwango kikubwa,ndani na nje ya nchi,huku ukamuaji wake
ukitegemea viwanda vidogo vidogo vinavyoweza kumilikiwa hata na Mkulima Mmoja.
“ Zao hilo limekuza kwa kasi uchumi wa
mkoa wa Singida,kutokana na bidhaa yake kuhitajika kwa wingi,na utengenezaji
wake hauhitaji mitambo mikubwa,sasa mkoa wa Shinyanga una ardhi bora zaidi,ni
imani yangu utafanya vyema zaidi ya Singida,”alisema Ntelya.
Aidha alisema pindi Wakulima
wakililima zao hilo kama la biashara itasaidia kwa kiwango kikubwa kwa
Mwekezaji wa Kiwanda cha Mafuta ya Alizeti cha Mkoani Shinyanga ambacho
uzalishaji wake unakabiliwa na changamoto ya malighafi za kutosha.
Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa wa
Shinyanga,Zainab Telack,katika ziara yake ya kikazi wilayani Kahama,aliwaasa
Madiwani na Wabunge,kuwahamasisha wakulima kuzalisha malighafi ambazo
zitaongeza thamani ya kilimo chao na kuuza katika viwanda vya wawekezaji
waliopo Mkoani Shinyanga.
Alisema Wawekezaji waliopo mkoani
Shinyanga,wanakabiliwa na changamoto za malighafi ili kumudu kuendesha shughuli
zao walizowekeza,hivyo ni jukumu la wakazi wa Mkoa wa Shinyanga,kunufaika kwa
kukuza uchumi wao na Taifa kwa ujumla kwa kuzalisha malighafi zitakazokuwa na
tija kwa Mwekezaji.