Tuesday, June 20, 2017

MAKINIKIA YAWAIBUA WAZEE KAHAMA,WAZISHANGAA HALMASHAURI ZAO.

BOFYA HAPA CHINI KUONA MAAJABU YA LEO




UMOJA wa Wazee wilayani Kahama(UWAKA),umeibuka na kumpongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,John Pombe Joseph Magufuli,juu ya hatua alizochukua kuhusiana na kufichua ufisadi uliokuwa ukifanyika katika mchanga wa dhahabu ( Makinikia
),baada ya kuona Halmashauri zao zinachelewa kutoa pongezi.

Aidha Uwaka umezishangaa  Halmashauri za Msalala na Mji zilizo wilayani Kahama,kwa kushindwa kujitokeza kumpongeza Rais Magufuli,kuwafichua wanaotorosha mchanga wa madini(Makinikia),ilhali Halmashauri hizo ndio waathirika wakubwa.

Wakiongea kwa masikitiko makubwa,katika kikao chao maalumu,Wazee hao wa Uwaka,walidai Halmashauri hizo mbili ndio waathirika wakubwa,hivyo walitaraji Mabaraza ya madiwani yangeitishwa  kwa vikao vya dharura,ili kuunga mkono juhudi za Rais na kumpongeza kwa kuwafichua mafisadi wa Makinikia.

Katibu wa Uwaka,Paul Ntelya,alisema alichokifanya Rais hakikutarajiwa na kimemgusa kila Mtanzania mzalendo mpenda Maendeleo kinastahili kupongezwa ili kumuunga mkono kwa jitihada za kuwafichua wezi wa mali za nchi.

“ Tulitegemea Halmashauri zetu hizi mbili,kupitia Mabaraza yetu,zingeliketi pamoja na kutoa tamko,maana kwa upande Bulyanhulu ilipo Halmashauri ya Msalala,imeathirika tangu mwaka 1998,huku Halmashauri ya Mji ulipo Mgodi wa Buzwagi wenyewe tangu 2001,huku zikiwa na madai yao lakini zimekaa kimya,”alisema Ntelya.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Uwaka,Bathlomew Kayoka,alisema Halmashauri hizo zilistahili kuitisha mabaraza ya dharura yenye vimelea vya uzalendo,kutoa pongezi kwa niaba ya wananchi wa maeneo hayo ambao hawanufaiki na huduma za jamii  kutoka migodi hiyo kulingana na thamani ya mali wanayovuna.

“ Sisi wazee hili limetugusa na kutusisimua sana,kwani limetoa matumaini ya maendeleo chanya kwa jamii yetu,ama hakika tuna Rais mzalendo,hivyo kwa niaba ya wana Kahama,tumedhamiria kufikisha pongezi zetu hizo kupitia kwa Mkuu wa wilaya ya Kahama,”alisema Kayoka.

Nae Mzee Deogratias Mulumba,alisema pamoja na kutoa pongezi hizo,wana Kahama hawana budi kushinikiza Kampuni ya Acacia kuwajengea vyuo vitatu vyenye hadhi,ambapo alianisha vyuo hivyo kuwa ni budi kiwepo cha VETA,Afya na Elimu,hatua itakayosaidia wakazi wa eneo hilo kuona wamenufaika japo kidogo kuwepo kwa Mwekezaji huyo.

Hata hivyo Mwenyekiti wa Halmashauri ya Mji wa Kahama,Abeli Shija,akiongea kwa njia ya simu na gazeti hili,alidai waliita baadhi ya vyombo vya habari(Hili halikuwa katika Mwaliko)na kutoa tamko la kumpongeza Rais Magufuli,siku hiyo hiyo alipokabidhiwa taarifa ya pili ya Uchunguzi juu ya Makinikia.

KUONA VIDEO MPYA BOFYA HAPA CHINI