WANANCHI wa Kata ya Lunguya katika Halmashauri
ya Msalala,Wilayani Kahama Mkoani Shinyanga,wamelalamikia tozo za Ushuru
mbalilmbali wanazoshinikizwa kulipa na
maafisa wa biashara katika
Halmashauri yao.
HIvyo wamemuomba mbunge wa Jimbo hilo,
Ezekiel Maige,awasaidie kutatua kero hiyo ambayo inawadhoofisha kiuchumi
kutokana na kulazimika kulipa ushuru
usiozingatia mfanyabiashara mdogo ama mkubwa,anaandika Michael Francis Bundala.
Wakizungumza mara baada ya mbunge huyo
kutembelea katika kitongoji cha Nyangarata,Vijiji vya Kalole na Kabanda,
wamemuomba mbunge huyo kuchukua hatua za makusudi ili aweze kuwasaidia.
Wamesema licha ya Rais Magufuli
kukataza ushuru kwa wafanyabiashara wadogo lakini halimashauri hiyo inaendelea
kutoza ushuru kwa wafanyabiashara wadogo na mama lishe na bila kuzingatia
kiwango cha mtaji cha kila mfanyabiashara au mama lishe.
Hilda Julius mkazi wa Kata ya Lunguya,amehoji
vipi mchuuzi wa mchicha unaotembezwa katika beseni atozwe kodi ya Shilingi Elfu
Kumi na tano kwa mwezi,ilhali kipindi cha Kampeni Rais John Magufuli,alinadi
ilani ya CCM kwa kueleza kutotozwa kodi ndogo ndogo?
Nae Nae Petro Shaba Madiba anasema
hawapingi kulipa ushuru kwakuwa wanatambua ni wajibu wao lakini wanachokipinga
ni kutozwa ushuru mkubwa usiolingana na kipato chao ama ukubwa wa biashara,huku
wakilazimika kulipa kiwango kinacholingana na wenye biashara kubwa jambo
analodai ni kuwaumiza wafanyabiashara wadogo.
Kufuatia malalamiko hayo Mbunge wa Jimbo
la Msalala,Ezekiel Maige, amewaahidi wananchi hao kulishughulikia suala hilo
mapema iwezekanavyo kwa kuwa linakiuka kile kilichozungumzwa na Rais wakati wa
kampeni za uchaguzi mwaka 2015.
“…ushuru umebaki kwa wafanyabiashara
wanaosafirisha mazao na si kwa wanaouza ili wajikimu kimaisha,boda boda na
wauza mchicha ushuru umekatazwa kwa mujibu wa maelekezo ya Rais Magufuli,lakini
hapa kuna mkanganyiko,hivyo ntalishughulikia na mtaletewa muongozo kamili na Halmashauri unaofafanua
hayo maelekezo ya Rais.”Anasema Maige.
Kwa upande wake Diwani wa Kata hiyo,Benedict
Manuali,amesema suala la ushuru limekuwa na mkanganyiko mkubwa katika kata hiyo
ambapo wananchi wa eneo hilo wamekuwa wakilalamika kutozwa ushuru ambao
hauangalii mtaji wa mfanyabiashara.
Manuali anasema,“malalamiko hayo pia
aliwahi kuyapata toka kijiji cha Kalole,ambapo mama lishe,wauza mbogamboga
wanakumbana na kero hiyo,niliiwasilisha kwa Mkurugenzi ambaye aliahidi kutuma
wataalamu kuja kuwaelimisha ikiwemo matumizi ya mashine za kietroniki za
kutozea kodi,lakini hakuna lililofanyika.”
Katika hatua nyingine Mbunge wa jimbo
hilo ametoa mifuko 100 ya saruji katika kitongoji cha Nyangarata kwa kuwa
wananchi wa eneo hilo wamekubaliana kujenga shule kwa nguvu zao wenyewe ili
watoto wao wapate shule na waepukane na suala la watoto wao kusafiri umbali
mrefu kwenda kusoma.
KUONA VIDEO MPYA BOFYA HAPA CHINI