KITENDO cha Serikali ya awamu ya tano,kuzuia Mchanga kutoka
eneo la
madini,kusafirishwa nje ya nchi,kimepongezwa kuwa cha
Kizalendo,kilichopaswa kudhibitiwa kipindi kirefu.
Maamuzi hayo yanastahili kuungwa mkono kwakuwa yanaokoa
rasilimali,iliyosafirishwa nje ya nchi kwa kumnufaisha Mwekezaji pasipo kuwa na
tija kwa Taifa la Tanzania,anaandika Michael Francis Bundala.
Baadhi ya Wananchi wa kijiji cha Kakola,Kata ya Bulyanhulu katika
Halmashauri ya Msalala,wilayani Kahama,wamefurahishwa na maamuzi hayo na kudai
wapo tayari kuandamana mwendo mrefu kuunga mkono juhudi za Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dk John Pombe Magufuli za kuzuia mchanga
kusafirishwa nje ya nchi.
Shauku yao hiyo wameileza katika mkutano wa hadhara,walipotembelewa
na Mbunge wa Jimbo la Msalala,Ezekiel
Maige,kusikiliza kero zao,ambapo walimpongeza Rais Magufuli kwa madai amefanya
jambo muhimu walilokuwa wakilisubiri.
Wakieleza kero zao kwa mbunge huyo wamesema wamechoshwa na
unyonyaji unaofanywa na mgodi wa dhahabu wa Bulyanhulu,unaomilikiwa na Kampuni
ya ACACIA,uliopo katika kata yao,umekuwa ukitoa ahadi za kusaidia maendeleo kisha baadaye kushindwa kutekeleza,hivyo kuzuia mchanga
kusafirishwa nje ni hatua nzuri iliyofanywa na Rais.
Mwenyekiti wa Kijiji cha Kakola,Emmanuel Bombeda,amesema
usafirishaji mchanga huo umenufaisha baadhi ya watumishi mgodini,ambao ni
Watanzania ambao hawana mioyo ya kizalendo zaidi ya kuangalia maslahi yao
binafsi.
Anasema,“ tunaunga mkono kwa Rais Magufuli kuzuia wizi huo,kwani
tunaushahidi wa asilimia 99 watu hao ni wezi kwa kusafirisha mchanga huo ambao
ungelibaki ungelinufaisha wachimbaji wadogo wadogo wanaopatikana katika kijiji
cha Kakola.”
Mkazi wa Kijiji cha Kakola,Albert Wakati Sagembe,amesema
tatizo kubwa la Mgodi huo kutokuwa na Meneja Uhusiano kutoka Kanda ya
Ziwa,ambaye angelikuwa na uchungu kwa kuhakikisha anasimamia maendeleo stahiki
ya eneo lililo pembezoni na Mwekezaji.
Mbunge wa jimbo hilo, Ezekiel Maige amesema yupo pamoja na
wananchi hao na watakapotaka kuandamana atashirikiana nao kuomba kibali cha kufanya maandamano ya amani
kwa kuwa Mgodi huo wa Bulyanhulu umekuwa hautekelezi majukumu yake kwa
wananchi.
“….walituahidi kutuboreshea miundo mbinu ya barabara huduma
za jamii hapa Kakola kama afya,elimu na maji,ambayo haijatekelezeka,kwa ujumla
hawana mkakati mzuri wa kusaidia maendeleo jambo ambalo wameonesha si
waungwana,kwa kuahidi pasipo kutimiza.”Anasema Maige.
Aidha Mwenyekiti wa kijiji hicho,Bombeda amemshukuru mbunge huyo kwa kufika katika
eneo hilo kusikiliza kero za wananchi na kumuomba mbunge huyo kuyafanyia kazi
malalaniko ya wananchi kuhusu mgodi wa Bulyanhulu.
KUONA VIDEO MPYA BOFYA HAPA CHINI