WATUMISHI wa
Kitengo cha Ardhi na Mipango Mji katika Halmashauri ya Mji wa Kahama,ambao
wamehudumu kwa kipindi kirefu,wametakiwa kuhama kutokana na kubainika kuwa
ndio
chanzo cha kukithiri kwa migogoro ya Ardhi.
Imedaiwa
utumishi wao kwa kipindi kirefu,katika Halmashauri ya Mji wa Kahama,kumewapa
ujasiri wa kutekeleza majukumu yao kwa maslahi binafsi pasipo kujali
wanazalisha migogoro ya Ardhi inayokosa utatuzi,ambayo imekuwa kero kwa wakazi
wa Kahama.
Tuhuma hizo
zimebainishwa katika Kikao kawaida cha Baraza la Madiwani wa Kahama kilichokaa kwa lengo la kujadili
taarifa ya robo ya tatu ya shughuli za utekelezaji za Halmashauri hiyo
zilizofanyika katika kipindi hicho,huku likitolewa pendekezo la kuhamisha
watumishi hao ambao wamekuwa hawana tija katika Halmashauri hiyo.
Katika Kikao
hicho,Madiwani walimshauri Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Mji wa Kahama,kufanya
mchakato wa kuiomba Tamisemi kuwahamisha watumishi hao,kutokana na kuhudumu kwa
kipindi kirefu katika Mji wa Kahama,huku wakisababisha kuongezeka kwa migogoro
ya ardhi katika Mji huo.
“Kwa nini hawa
watumishi wa Idara ya Ardhi na Mipango Miji wasibadilishane na wale wa
Shinyanga, Washinyanga waje Kahama na hawa wa Kahama waende Shinyanga kwani kunashindikana
nini? Hawa wamekaa muda Mrefu hapa na ndio wanaosababisha migogoro isiyoisha ya
ardhi hapa Mjini”, Alihoji Diwani wa Viti Maalumu,Kata ya Kahama Mjini,Aoko
Nyangusu.
Madiwani hao
walimtaka Mkurugenzi wa Halmashauri hiyo kuhakikisha anakamilisha
mchakato wa kuwakataa na kuwahamisha watumishi hao mapema iwezekanavyo,kinyume
cha hapo wametishia kufikia maazimio ya kumkataa Mkurugenzi huo,hali ambayo
italeta mkanganyiko mkubwa katika Halmashauri hiyo ya Mji.
Aidha Diwani
huyo aliomba kama kuna kanuni inayomzuia Mwenyekiti wa Halmashauri ya Mji
kuhudhuria vikaao vya Kamati ya Ardhi na Mipango Mji,itenguliwe ili apate fursa
ya kuhudhuria,hatua itakayosaidia kutatua kwa haraka migogoro hiyo ya ardhi
ambayo imekuwa changamoto kubwa ya Maendeleo katika Mji wa Kahama.
Kwa upande
wake Mwenyekiti wa Halmashauri ya Mji wa Kahama Abel Shija alisema kuwa
kwa sasa Halmashauri yake imejitahidi kwa kiasi kikubwa kutatua migogoro
ya ardhi iliyokuwepo hapo zamani na kuongeza kuwa kwa sasa hali imekuwa
tofauti kwani migogoro imepungua kwa kiasi fulani kwa Wananchi.
“Kwa sasa
migogoro ya ardhi iliyokuwepo hapo zamani imepungua kwa kiwango kikubwa,hapo
awali Maafisa ardhi walikuwa wakigawa kiwanja kimoja kwa watu karibuni saba na
kuleta mvutano huku Halmashauri ikipata lawama kubwa kutoka kwa Wananchi wa mji
wa Kahama,sasa hali hiyo haipo”. Alisema Mwenyekiti wa Halmashauri ya Mji wa
Kahama.
Nae Katibu
Tawala wa Wilaya ya Kahama Timoth Ndanya alisema kuwa Migogoro ya ardhi
katika Mji wa Kahama ni mingi na kuwataka madiwani na watumishi wa Halmashauri
hiyo kushirikiana kuitatua huku wakihakikisha haizaliwi migogoro mingine.
Kikao hicho
cha Baraza la Madiwani kiliamua kuunda Kamati ya kuchunguza na kufuatilia
migogoro ya ardhi katika Halmashauri hiyo,pamoja na maeneo ya makaburi
yaliyovamiwa kujengwa nyumba za makazi,ikiwa ni kamati ya pili kuundwa kwani
awali Mkuu wa Wilaya ya Kahama
alishaunda Kamati kwa ajili ya kufuatilia suala hilo.
KUONA VIDEO MPYA BOFYA HAPA CHINI