IDARA ya Usafi na
Mazingira Kata ya Isaka,wilayani Kahama,imeshutumiwa kushindwa kuwajibika kusimamia usafi,kutokana na taka ngumu
zinazokusanywa kutupwa katika eneo lililotengwa kwa ajili ya Madhehebu ya dini,
kuzika watu wao waliofariki.
Tuhuma hizo zimewasilishwa
na wajumbe wa Kamati ya Maendeleo ya Kata,katika kikao chao maalumu ambapo
wamedai kushangazwa kuona taka ngumu zinazozalishwa majumbani, kutupwa katika eneo
lililo maalumu kwa ajili ya kuzika watu waliofariki.
Mjumbe wa Kamati ya
Maendeleo ya Kata hiyo,Khalfan Sultani,alihoji umuhimu na uwajibikaji wa Idara
hiyo iwapo eneo hilo takatifu likichafuliwa kwa kutupiwa taka ngumu.
MJUMBE Khalfan Sultan akichangia mada. |
“ Wenzetu wamezikwa na
sisi tuko nyuma yao kwahiyo mimi ninaiomba Serikali ihakikishe inazuia kupeleka
takataka eneo hilo,lakini pia itafute eneo maalumu lakuweza kupeleka takataka hizo kuliko makaburini.”Alisema Sultani.
Hata hivyo Afisa Afya wa
Kata ya hiyo ya Isaka;Elias Nchunga,alishtushwa kutendeka kwa jambo hilo ambalo
hata hivyo,alidai,kutokuwa na taarifa nalo na kuahidi kulifuatilia kisheria kwa
watakaobainika na uchafuzi huo wa mazingira katika eneo la makaburi.
“ Kama anatokea mtu wa
jinsi hiyo anayechafua makaburi kwakweli anakwenda kinyume cha taratibu,kanuni
n sheria za nchi,na kwa maana ingine nitakachokifanya ni kufuatilia kupata
uhakika wa hilo jambo halafu na kuona
yupi anayehusika katika hili.”
DIWANI wa Kata ya Isaka,Dkt.Gerald Mwanzia akiongea. |
Kwa upande wake Diwani wa
Kata hiyo,Dkt.Gerald Mwanzia,amesema kwa kipindi kirefu Kata haikuwa na
dampo,na ndio sababu ya kutokea vitendo hivyo ambavyo amekiri si vya kiungwana
kwa badhi ya jamii kwenda kutupa taka katika eneo hilo muhimu kwa ajili ya
maziko ya marehemu wa dini mbalimbali.
AFISA Maendeleo wa Kata ya Isaka,Grace Nyahonge akichangia hoja. |
Dkt.Mwanzia alisema
kutokana na kuona umuhimu wa suala hilo tayari amelipatia ufumbuzi kupitia
Halmashauri ya wilaya ya Msalala,hivyo kusikitishwa na kitendo hicho kwakuwa
tayari eneo la kuhifadhi taka limeishatengwa na kutaka Maafisa watendaji wa
Kata na Vijiji kulifanyia kazi kwa kutoa maelekezo kwa jamii.
“Sisi kama Kata tayari
tumeishapata eneo la kuhifadhi taka,sasa hatutarajii tena kuona kwamba takataka
zinapelekwa makaburini na itabidi Watendaji wote kwa pamoja waweze kuona kwamba
wanaweka udhibiti matangazo pale katika eneo la makaburini ilikusitisha watu
wote kuweza kutupa uchafu katika eneo la makaburini bali takataka hizo zote
zielekezwe katika sehemu ambayo tayari Halmashauri ya wilaya imelinunua kwa
ajili ya shughuli hiyo,”alisema Dkt.Mwanzia.
BAADHI ya Wajumbe wakiwa katika Kikao hicho. |
Kikao hicho cha Kamati ya
Maendeleo ya Kata,mbali na kuibua kero hiyo ya uchafu,pia kiliadhimia kwa kauli
moja kuanzisha Mfuko wa Maendeleo ya Kata,ambao utasukuma mbele maendeleo
katika sekta ya Elimu na Afya pamoja na kuweka mikakati ya ulinzi na usalama
kwa wakazi wake kutokana na kuwa kituo cha biashara kinachokusanya
wafanyabiashara wa ndani na nje ya nchi.