MKUU wa Mkoa wa Simiyu,Anthony
Mtaka,amemsimamisha kazi Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya wilaya ya
Itilima,John Aloyce kutokana na kukabiliwa na tuhuma mbalimbali
ikiwemo kushindwa kuisimamia halmashuari hiyo na kusababisha kuwepo kwa
migogoro ya mara kwa mara kati ya madiwani na watendaji.
Mkuu huyo wa Mkoa alichukua maamuzi
hayo katika kikao cha dharura cha Baraza la Madiwani kilichofanyika jana mjini
Langangabilili wilayani humo,ambapo pia amefuta posho zote kwa wakuu wa idara
na vitengo katika halmashauri zote zilizoko mkoani humo wanaoingia katika vikao
vya madiwani.
Alibainisha posho alizofuta ni za
kwenye Vikao vya baraza na kamati za halmashauri kwa madai kuwa hazina tija
yoyote, na kuamuru fedha hizo zilizotengwa zifanye kazi nyingine za maendeleo
kama vile utengenezaji wa madawati.
MKUU wa Mkoa wa Simiyu akitoa maamuzi . |
Katika kikao hicho madiwani hao
walisema serikali ilitoa Sh milioni 450 kwa ajili ya ujenzi wa nyumba za
watumishi katika halmashauri hiyo lakini kazi hiyo haikufanyika, wanapohoji na
kutoa uamuzi umekuwa haufanyi kazi.
“Wilaya yetu ni mpya na katika
kuondoa tatizo la watumishi wa halmashauri hii kuishi mbali na makao makuu ya
wilaya tuliamua kuanza ujenzi wa nyumba za watumishi na tukaletewa Sh milioni
450. Lakini kila tunapohoji matumizi ya fedha hizo hatupatiwi majibu na
tunapomwagiza Mkurugenzi atuletee hakubaliani na maamuzi yetu,”alisema Kuzenza
William (CCM), ambaye ni Diwani wa Kata ya Zagayu.
Walisema kuwa hata mapato ya ndani
yanayopatikana hayafahamiki licha ya kuwepo kwa ushuru wa mazao mchanganyiko
haulipwi na wafanyabiashara walio wengi, hivyo kusababisha shughuli nyingi za
halmashauri kukwama na kuzua migogoro ya mara kati ya madiwani na ofisi ya
Mkurugenzi.
“Mapato ya ndani hayafahamiki kabisa
kuwa ni kiasi gani cha fedha kimepatikana, maana hatusomewi na inaonekana hata
ushuru wa mazao mchanganyiko wafanyabiashara hawalipi hii timu ya mkurugenzi
inayosimamia mapato sina imani nayo,” alisema Diwani Kata ya Lugulu, Robert
Jongela.
Mwenyekiti wa halmashauri hiyo, Daud
Nyalamu alisema madiwani wa halmashauri hiyo wanaonekana hawana uamuzi kwani
waliagiza kuwa vifaa vyenye thamani ya Sh milioni 320 vilivyokopwa na
halmashauri hiyo kwa ajili ya ujenzi wa maabara 35 za shule za sekondari
vifanye kazi, lakini hadi sasa hakuna kilichofanyika na vingi vimeharibika.
“Tulikopa benki Sh milioni 320 kwa
ajili ya ujenzi wa maabara 35 zilizoko katika halmashauri yetu, vifaa
vimenunuliwa lakini hadi sasa vimesambazwa maeneo mbalimbali havijafanyiwa
kazi. Vimeharibika kwani saruji imeganda na mbao zimepinda na hazifai kwa
ujenzi. Hii inatokana na uzembe wa Mkurugenzi wetu na kila kukicha halmashauri
inadaiwa hadi madiwani hatulipwi stahili zetu,” alisema.
Akizungumzia tuhuma dhidi yake,
Aloyce alisema tangu ateuliwe kuwa Mkurugenzi wa halmashauri hiyo miezi sita
iliyopita alikuta Sh milioni 126 zilizokuwa zimebaki katika ujenzi wa nyumba za
watumishi.
“Mimi wakati nafika katika
halmashauri hii nilikuta kati ya Sh milioni 450 za ujenzi wa nyumba za
watumishi zilikuwa zimebaki Sh milioni 126, tulikaa na wakuu wa idara tukaamua
tuzikope na kujenga ukumbi ukizingatia ya kuwa tulikuwa tunaelekea uchaguzi
mkuu hivyo tungeshindwa mahali pa kukusanyia matokeo ya kura,” alisema.
Alisema licha ya tuhuma mbalimbali
dhidi ya halmashauri hiyo, iliundwa tume kutoka Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Simiyu
kuzichunguza lakini hadi sasa hawajawaletea majibu, hivyo kuomba iundwe tume
huru kutoka nje ya mkoa ili kuweza kuzichunguza tuhuma zilizotajwa na madiwani
dhidi yake na ikibainika yuko tayari kuachia ngazi.
KUONA VIDEO MPYA BOFYA HAPA CHINI